Wito umetolewa kwa vijana wote nchini kuiga mfano wa GN Entertainment Group kutumia vipaji walivyonavyo katika sanaa ili kujipatia ajira na maisha bora ili kulikomboa taifa kutokana na wimbi kubwa la vijana wasio na ajira.Wito huo umetolewa jana na Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Mhe. Dkt. Milton Makongoro Mahanga alipokuwa akizindua filamu ya My Enemy ya GN Entertainment Group ya mjini Shinyanga.
Dkt. Mahanga amekipongeza kikundi hicho cha sanaa kwa juhudi zao za kuhamasisha vijana kufanya kazi za kujiajiri wenyewe badala ya kujihusisha na vitendo viovu.Kupitia filamu hiyo, vijana hao wamekuwa wakitoa na kuendelea kutoa ushauri na hamasa kwa vijana ili waweze kuwa wabunifu na kujiajiri na kuachana na vitendo viovu vya ujambazi, matumizi ya madawa ya kulevya na kuachana na matendo yanayoweza kuwasababishia maambukizi ya virusi vya UKIMWI na UKIMWI wenyewe.
Dkt. Mahanga amewashukuru vijana wa kikundi hicho kwa kuisaidia Serikali katika suala zima la ukuzaji ajira. “Niseme tu kwamba elimu hii mnayoitoa na mtakayoendelea kuitoa kupitia filamu zenu, kwa kweli ni kuisaidia Wizara yangu kazi yake, kwani kauli mbiu ya Wizara yangu katika suala zima la vijana na ukuzaji wa ajira kwa vijana ni pamoja na kutoa elimu kwa vijana kuhusiana na suala zima la ajira kwa vijana na kuachana na vitendo viovu”.
Katika kukiunga mkono kikundi hicho cha sanaa, Wizara ya Kazi na Ajira ilichangia shilingi milioni moja. Kikundi hicho kinahitaji jumla ya shilingi milioni 15 ili kufikia malengo waliojiwekea ambayo ni pamoja na ununuzi wa vitendea kazi mbalimbali.
No comments:
Post a Comment